![](https://swahilitimes.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/WhatsApp-Image-2025-02-06-at-05.33.19.jpeg)
Muungano wa Alliance Fleuve Congo (AFC), ambao una uhusiano na waasi wa M23 umeunda Serikali mpya nchini DRC kwa kumteua Kanali Bahati Musanga kuwa Gavana wa Jimbo la Kivu Kaskazini, manaibu Gavana wawili, Willy Manzi na Shadary Bahati, Meya wa Jiji la Goma, pamoja na Wakuu wa Wilaya.
Uteuzi huo umetangazwa wiki moja baada ya kuuteka mji wa Goma, huku sehemu kubwa ya maeneo mengine likiwemo eneo kubwa ya Walikale, Lubero, na Beni yakiwa bado chini ya udhibiti wa serikali ya DRC.
Serikali ya DRC bado haijatoa tamko lolote kuhusu hatua hiyo wakati ambapo hivi karibuni ilimteua Meja Jenerali Somo Kakule kuwa Gavana mpya wa kijeshi wa Kivu Kaskazini.
Kakule, ambaye kwa sasa anaendesha shughuli zake kutoka mji wa Beni, amesema kwamba lazima achukue mji wa Goma, ambako kuna ofisi kuu ya Gavana.
Umoja wa Mataifa (UN) unadai kuwa M23 inasaidiwa na Rwanda na inanufaika kupitia biashara haramu ya madini ya thamani kutoka migodi inayodhibitiwa na kundi hilo, hususan coltan kutoka migodi ya Rubaya, ambayo ni miongoni mwa migodi mikubwa duniani inayozalisha madini hayo.
M23 imekanusha madai ya uchimbaji na biashara ya madini katika maeneo inayoiteka na pia inakana kupokea msaada kutoka Rwanda.