Vurugu zimetokea ndani ya ukumbi wa Bunge la Ghana wakati wa mjadala kuhusu pendekezo la serikali la kuweka tozo kwenye miamala ya kielektroniki.
Wabunge hao wamefikia hatua ya kushikana mashati, kusukumana, kurushiana ngumi na viti wakati wengine wakiwa waamuzu wa ugomviu huo.
Ugomvi ulianza baada ya wabunge wa upinzani kukimbilia mbele na kumzuia Naibu Spika, Joseph Osei Owusu kutoka kwenye kiti chake kwenda kupiga kura. Kufuatia vurugu hizo, alilazimika kuahirisha kikao hicho kutokana na kukiukwa kwa taratibu.
Chama cha upinzania, National Democratic Congress (NDC) kinapinga pendekezo la tozo ya asilimia 1.75 kwenye miamala ya kielektroniki ambayo pia inajumuisha miamala kwa njia ya simu.
Wanapinga uamuzi huo kwamba utawagharimu watu wa kipato cha chini na watu walio nje ya mfumo rasmi wa kibenki.
Hata hivyo, Waziri wa Fedha, Ken Ofori-Artta amesema ni muhimu kupanua vyanzo vya mapato na kwamba mpango huo utaweza kuipatia serikali TZS trilioni 2.6 mwaka ujao.
Vurugu zimekuwa sehemu ya bunge la nchi hiyo ambapo mapema Januari mwaka huu wanajeshi walilazimika kuingia ndani ya Bunge kumaliza vurugu wakati wa uchaguzi wa spika.
Baadhi ya raia nchini humo wamekosoa vurugu huzo na kusema kuwa wabunge wao wanatakiwa kuwa watu wakuigwa, na sio kutenda mambo kwa namna isiyofaa.