Wabunge wa CCM: Halitokuwa bunge la kupiga makofi

0
42

Mbunge mteule wa Makete (CCM), Festo Sanga amesema wabunge wa CCM hawatakwenda kupiga makofi bungeni na badala yake watakosoa kistaarabu.

Akizungumza katika viunga vya bunge mara baada ya kufanya usajili amesema, “hatutakwenda kupiga makofi. Kaulimbiu ya Rais Dkt. Magufuli inasema ‘Hapa Kazi Tu,’ hii ni Serikali ya kazi, waziri asiyefanya kazi hatutampigia makofi, tutapaza sauti kuliko wale waliokua wakipinga miradi ya maendeleo.”

Naye mbunge mteule wa viti maalum (CCM) Mkoa wa Kagera, Neema Lugangira amewataka wapinzani waheshimu maamuzi ya wananchi.

“Tuheshimu maamuzi ya wananchi, dhana ya kusema Bunge hili halitakosoa ni dhana inayolenga kutudhoofisha, nitakosoa, ni jukumu langu kuwasemea wanawake na mashirika yasiyo ya Serikali kwa sababu ndio walionituma.”

Mbunge mteule wa Kikwajuni (CCM), Hamad Masauni amesema wabunge wanaotokana na CCM ndio waliokua wakitoa michango iliyoisaidia Serikali ya Awamu ya Tano, hivyo wananchi wapuuze propaganda za wapinzani zinazodai kuwa bunge la 12 halitaikosoa Serikali.

“Hata katika bunge lililopita michango mingi iliyokua ikiisaidia serikali ni ya wabunge wa CCM, wabunge wa CCM hawasusii bajeti, wabunge wa CCM hawatoki nje wakafunga midomo yao, wabunge wa CCM hawapingi miradi ya maendeleo au leo hawasemi hiki kesho wakasema kile, wana misimamo isiyoyumba,” amesema Masauni.

Bunge la 12 linatarajiwa kuanza kesho Novemba 10, 2020 ambapo miongoni mwa mambo yatakayofanyika katika mkutano huo wa kwanza ni kuchagua spika na naibu spika, kumthibitisha waziri mkuu, kusomwa kwa tangazo la Rais la kufungua bunge.

Send this to a friend