Wadau: Bila D 5 huwezi kusomea Ufamasia

0
53

Katika kuboresha huduma za afya nchini, wadau katika sekta mbalimbali wameazimia kuboresha mtaala wa kozi ya ufamasia kwa kuboresha kigezo cha kujiunga na vyuo vya kati vinavyowataka wanafunzi kuwa na ufaulu wa elimu ya Sekondari kwa alama D tano za masomo ya Fizikia, Baiolojia, Kemia, Kiingereza na Hisabati kutoka alama D mbili za Baiolojia na Kemia kama ambavyo ilivyo sasa.

Hayo yamebainishwa katika Kikao kilichowakutanisha wadau wote wa mitaala ya mafunzo kwa vyuo vya kati kutoka Serikalini, mashirika ya kidini, vyuo vya kati, vyama vya kitaaluma, wahitimu, watoa huduma, waajiriwa, Chama cha Wamiliki wa Vyuo vya Kati (APHECOT) na wamiliki wa vituo vya kutolea huduma za Afya.

Aidha, wadau hao wameshauri vigezo hivyo ambavyo pia vimeazimiwa kutumika katika udahili wa kozi za uuguzi na ukunga vioane na nchi jirani, na Afrika kwa ujumla na vizingatie usalama wa wananchi kwani wataalamu watakaozalishwa watakwenda kutoa huduma za afya zinazohitaji umakini mkubwa.

Wadau wengi wameeleza kuwa lengo la kufanya hivyo ni kuzalisha wataalam wenye sifa stahiki kwa ajili ya kuweza kusoma taaluma ya famasia na baadaye kuweza kutoa huduma bora kwa wananchi.

Wameongeza kuwa usalama wa wananchi katika huduma za afya ni kipaumbele kikuu kwa kuwa wataalamu hao wanaenda kutoa huduma za afya ambapo kwa kufanya kosa dogo linaweza kuleta madhara makubwa ikiwemo vifo.

Send this to a friend