Wadukuzi wavamia mifumo ya Benki Kuu ya Uganda na kuiba mabilioni ya pesa

0
32

Wizara ya Fedha ya Uganda imethibitisha ripoti za vyombo vya habari kuhusu wadukuzi kuvamia mifumo ya Benki Kuu na kuiba fedha, lakini imekanusha madai kuwa kiasi kilichoibwa kilifikia dola milioni 17 [TZS bilioni 44.8].

“Ni kweli akaunti yetu ilidukuliwa, lakini si kwa kiwango kinachoripotiwa,” amesema Waziri wa Nchi wa Fedha, Henry Musasizi, akiongeza kuwa ripoti ya tukio hilo itakamilika ndani ya mwezi mmoja. “Ili kuepuka upotoshaji, baada ya uchunguzi wa ukaguzi na CID kukamilika, nitarudi hapa bungeni na kutoa taarifa.”

Benki Kuu ya Uganda imesema siku ya Alhamisi jioni kuwa inasubiri matokeo ya uchunguzi wa polisi kuhusu ripoti za habari zinazodai kuwa wadukuzi waliiba dola milioni 17 [TZS bilioni 44.8] kutoka kwa benki hiyo.

Kwa mujibu wa gazeti la New Vision linalomilikiwa na serikali, wadukuzi waliotambulika kwa jina la “Waste” walivamia mifumo ya TEHAMA ya Benki Kuu ya Uganda na kuhamisha fedha hizo kinyume cha sheria mapema mwezi huu.

Taarifa zimeeleza kuwa wadukuzi hao wanasemekana kuwa na makazi Kusini-Mashariki mwa Asia, na sehemu ya fedha hizo zimehamishiwa nchini Japan, huku ripoti zikibainisha kuwa zaidi ya nusu ya fedha zimeweza kurejeshwa kupitia juhudi za haraka za Benki Kuu.

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni ameagiza uchunguzi wa kina ufanyike mara moja.

Send this to a friend