Wafanyabiashara Kariakoo wakanusha kutangaza kufanya mgomo

0
52

Wafanyabiashara wa Soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam wamekanusha tangazo linalosambaa katika mitandao ya kijamii likieleza kuwa kutakuwa na mgomo kuanzia siku ya Jumatatu Juni 24 kutokana na changamoto zao kutosikilizwa na Serikali.

Akizungumza na Azam Media, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo, Hamisi Livembe amesema tangazo hilo halijatoka katika jumuiya hiyo na hawana taarifa juu ya nani aliyehusika kuandika ujumbe huo.

“Hatujafahamu ni nani ameandika kwakweli, lakini taarifa tulizozipata ni kwamba Serikali kupitia TCRA wanafuatilia wao kujua limetoka wapi, kwa sababu kwakweli halikutoka miongoni mwetu,” ameeleza.

Akizungumzia kuhusu kamati iliyoundwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuhusu changamoto za wafanyabiashara, amesema katika bajeti ya mwaka jana zilichukuliwa changamoto tisa kati ya 21, na zilizobakia Serikali iliahidi kuzishughulikia katika bajeti ya mwaka huu, lakini katika bajeti iliyosomwa bungeni hayakutajwa.

“Tulifanya press ya kulalamikia hicho kilichotokea nikiongoza na mimi mwenyewe siku ya tarehe 18. Baada ya ile press, tarehe 19 niliitwa, Serikali ilinipa mwaliko nikaenda Dodoma, tulifanya vikao vingi […] tumezungumza, nimerudi leo lakini pia nimeambiwa kutakuwa na kikao kingine Jumatatu na tumefikia hatua nzuri,” ameeleza.

Hamisi amewatoa hofu wafanyabiashara hao na kutoa uhakika wa kuendelea na biashara kama kawaida.

Send this to a friend