Wafanyabiashara takribani 150 wenye maduka katika Kituo Kikuu cha Mabasi Mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro, wamefunga maduka yao leo Jumanne, Julai 30, 2024, ili kushinikiza Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kuwapunguzia kodi ya pango.
Wafanyabiashara hao wamesema wamechukua hatua hiyo baada ya manispaa kushindwa kutekeleza ahadi ya kupunguza kodi ya pango waliyopewa awali.
Kwa mujibu wa wafanyabiashara hao, aliyekuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda, ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, aliwaahidi kupunguziwa kodi ya pango kwa shilingi 50,000 kwa kila kibanda alipofanya mkutano eneo hilo. Hata hivyo, hadi sasa ahadi hiyo haijatekelezwa, jambo ambalo limewalazimu kuchukua hatua ya kufunga maduka yao ili kushinikiza utekelezaji wa ahadi hiyo.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Moshi, Shaban Mchomvu, amefika stendi kuu na kuzungumza na viongozi wa wafanyabiashara hao. Mchomvu amewaomba wafanyabiashara kuwa na subira wakati wakisubiri kuwasili kwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Zephania Sumaye, ili kupata ufumbuzi wa changamoto hiyo.
Wafanyabiashara wameomba serikali ya wilaya kuingilia kati na kutatua tatizo hili haraka iwezekanavyo ili waweze kuendelea na shughuli zao za kibiashara bila kikwazo cha kodi kubwa ya pango kwani hali ya biashara zao imekuwa ngumu kutokana na kiwango kikubwa cha kodi wanacholipa.