Wafanyabiashara wadogo maarufu kama machinga wa Soko la Namba 68, linalofahamika kama Kilombero jijini Arusha, wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Mashaka Gambo, kwa juhudi za kutatua changamoto ya maji sokoni hapo, kupitia mradi wa uchimbaji wa kisima kipya ambacho kitasaidia wafanyabiashara hao kupata huduma ya maji safi na salama.
Wakizungumza sokoni hapo, machinga hao wameeleza kuwa upatikanaji wa maji ni muhimu sana kwa shughuli zao za kila siku, hasa kwa wafanyabiashara wa mamantilie, wauza matunda, na huduma zingine zinazotegemea maji.
“Mrisho Gambo amekuwa msikivu, ameweza kutuchimbia kisima ambacho kitatusaidia kunufaika kwa kutuwezesha kupata maji safi na salama kwa ajili ya kuendesha shughuli zetu, tuna mamantilie, tuna wauza matunda. Yote hii inahitaji maji,” ameeleza Salome Mollel, mfanyabiashara wa nguo za mitumba sokoni hapo.
Kwa miaka mingi, changamoto ya maji imekuwa kikwazo kikubwa kwa wafanyabiashara wa soko hilo. Walikuwa wakiuziwa maji kwa bei ya juu, ndoo kubwa ikiuzwa shilingi 200 na ndogo shilingi 150, hivyo wamemshukuru Rais Samia na Mbunge Gambo kwa kutatua changamoto hiyo wakitumaini bei ya maji itakwenda kuwa chini kwa kupunguza gharama zao za kila siku.
Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Mashaka Gambo, amesema kuwa anatambua changamoto zinazowakabili wafanyabiashara hao, ikiwemo ufinyu wa miundombinu, gharama kubwa za umeme, na changamoto za mikopo. Hata hivyo, alisisitiza kuwa kutatuliwa kwa changamoto ya maji ni hatua moja muhimu kati ya nyingi zinazolenga kuboresha mazingira ya biashara sokoni hapo.
“Tutahakikisha tunafanya ukarabati wa miundombinu, kuweka taa za barabarani, na kuboresha mazingira kwa ujumla ili kuwawezesha wafanyabiashara kufanya kazi katika mazingira bora na salama,” amesema Gambo.
Pia amewataka wafanyabiashara kushirikiana na viongozi wa soko ili kuhakikisha huduma ya maji inawanufaisha wote bila changamoto za matumizi mabaya au kuuza maji miongoni mwa wanufaika wenyewe.