Wafanyabiashara waruhusiwa kuingiza mbolea kukabili upungufu

0
68

Serikali imekiri kuwa kuna upungufu wa mbolea kwa ajili ya shughuli za kilimo nchini na kusema kama mkakati wa muda mfupi wamewaruhusu wafanyabiashara kuingiza bidhaa hiyo nchini, ili wakulima waweze kuendelea na kilimo bila changamoto yoyote.

Aidha, kuhusu mkakati wa muda mrefu, serikali ya awamu sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imebainisha kuwa inaendelea kuwavutia wawekezaji wajenge viwanda nchini, kwani kiwanda kimoja kilichopo (Minjingu) hakitoshelezi mahitaji.

“Tumefanya jitihada za kupata wawezekaji kutoka Burundi, na mimi nimepata fursa ya kwenda kukutana na mwekezaji kule kule Burundi. Tumezungumza, amekubali kuja hapa, na tayari tumempa eneo hapa jijini Dodoma na ameanza ujenzi wa kiwanda,” amesema Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Majaliwa amefafanua kwamba, kwa uzalishaji anaoufanya mwekezaji huyo nchini Burundi, akizalisha na hapa nchini, tatizo la mbolea litakwisha kabisa, na amewataka wakulima kutokuwa na hofu kwani Rais Samia ameona changamoto hiyo, na anakusudia kuhakikisha inakwisha kwa wao kupata mbole kwa bei nafuu.

Waziri mkuu ameyasema hayo leo bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa Mufindi Kusini, David Kihenzile ambaye alitaka kujua mpango wa muda mfupi na wa muda mrefu wa serikali kumaliza tatizo la upungufu wa mbolea ambalo ni kero kubwa kwa wananchi.

Send this to a friend