Wafanyakazi wa OYA wafikishwa mahakamani kwa kesi ya mauaji
Wafanyakazi wanne wa taasisi ya mikopo ya OYA wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kibaha kwa tuhuma za mauaji ya Juma Said Seif (45), mkaazi wa Kitongoji cha Mbagala Mlandizi mkoani Pwani yaliyofanyika Oktoba 7, mwaka huu.
Watuhumiwa hao ni Dastan John Charles (23), Christopher John Charles (23), Emmanuel Joshua Olala(24) wakazi wa Kilangalanga Mlandizi pamoja na Abdallah Felix Wendiliwe (32) mkaazi wa Janga Mlandizi.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kibaha, Emmaeli Lukumai amesema ushahidi wa kesi hiyo iliyosomwa kwa mara ya kwanza bado haujakamilika, hivyo kesi hiyo imehairishwa hadi Oktoba 30 mkwaka huu.
Aidha, watuhumiwa hao hawakupewa nafasi ya kujibu lolote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi ya mauaji huku watuhumiwa wote wakirudishwa rumande.
Inadaiwa siku ya tukio, watuhumiwa hao walifika nyumbani kwa Juma kwa lengo la kudai fedha za marejesho ya mkopo kwa mke wake aitwaye Khadija Ramadhani, na ndipo walipoelezwa kuwa mkewe hayupo lakini watuhumiwa hao walilazimisha kuingia ndani kwa nguvu huku wakimshambulia sehemu mbalimbali za mwili wake kwa kutumia fimbo.
Baada ya hapo marehemu alianguka chini na kupoteza fahamu kisha watuhumiwa walimbeba kwa kutumia gari lao ili wampeleke hospitali na alifariki akiwa anapatiwa matibabu katika kituo cha Afya cha Mlandizi.