Wafanyakazi duniani kote wakiungana kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi, Mei Mosi mwaka huu, watumishi hao nchini wanasubiri kwa hamu kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu mishahara yao.
Shauku hiyo inatokana na ahadi aliyoitoa Rais wakati wa maadhimisho hayo mwaka 2021 ambapo alisema mwaka huu atakuja na kifurushi maalum cha kupandisha mishahara ya watumishi ambayo haijapanda kwa miaka saba serikalini na miaka tisa sekta binafsi.
“Imekuwa ni vigumu kwangu kuongeza mishahara mwaka huu [2021]… Lakini niwahakikishie wafanyakazi wenzangu kuwa mwakani siku kama leo ninakuja na package nzuri ya kupandisha mishahara,” alisema Rais mwaka 2021.
Hata hivyo, licha ya kuwa hakupandisha mishahara alichukua hatua kadhaa kuboresha maslahi ya watumishi ikiwa ni pamoja na kuwapandisha vyeo/madaraja, kutoa ajira mpya zaidi ya 44,000, kufuta tozo ya 6% iliyokuwa ikitozwa na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu na kupunguza makato ya kodi kwenye mishahara kutoka asilimia 9 hadi asilimia 8.
Katika hotuba hiyo, Rais Samia alisema yeye kama mmoja wa wafanyakazi anatambua umuhimu wa kuboresha maslahi ya watumishi kwani maendeleo ya Taifa lolote ni matokeao ya juhudi za wafanyakazi.
Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi mwaka 2022 kitaifa yanafanyika jijini Dodoma ambapo mgeni rasmi ni Rais Samia Suluhu Hassan, na kaulimbiu ni Maslahi Bora, Mishahara Juu, Kazi Iendelee.