![](https://swahilitimes.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/Snapinst.app_479923826_18055800449086565_3755617832168508653_n_1080-905x613.webp)
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innnocent Bashungwa ameliagiza Jeshi la Magereza kusimamia kikamilifu mpango wa kuwapa ujuzi na mafunzo ya ufundi stadi wafungwa wanapokuwa gerezani na watakaohitimu mafunzo kutunukiwa vyeti vinavyotambuliwa na VETA wakati wanapomaliza vifungo vyao ili kuwajengea uwezo wa kujitegemea wanaporudi uraiani.
Amesema hayo wakati wa ziara ya kikazi Makao Makuu ya Jeshi la Magereza, Dodoma ambapo amebainisha kuwa mpango huo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa Jeshi la Magereza wa kuwapa ujuzi wa ufundi stadi wafungwa pamoja na vyeti.
“Mheshimiwa Rais alitoa maelekezo kwa Kamishna Jenerali wa Magereza, kuwapa ujuzi (ufundi stadi) kwa kuwaendeleza wanaoingia gerezani na ujuzi, lakini wale wanaoingia hawana ujuzi kabisa, kuangalia namna ya kuwapa ujuzi ili wanapotoaa waweze kujikimu kimaisha,” ameeleza Bashungwa.
Aidha, Bashungwa amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuliboresha Jeshi la Magereza kwa kulipatia vifaa na vitendea kazi ikiwa ni pamoja na mabasi saba ya kusafirisha mahabusu.