Wagombea wa CCM watakiwa kuomba ruhusa kabla ya kuondoka majimboni

0
37

Wakati vyama mbalimbali vikiendelea na kampeni za kunadi sera zao kwa wananchi kuelekea Oktoba 28, 2020, Chama cha Mapinduzi (CCM) kimepiga marufuku wagombea wake kutoka majimboni mwao pasi na idhini ya Kamati ya Siasa ya Wilaya ya chama hicho.

Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Bashiru Ally ametoa maagizo hayo kupitia ukurasa wa Twitter wa chama hicho, huku akiwataka wagombea kufuata ratiba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na kamati za siasa.

“Tuwatafutie kura wagombea udiwani na mgombea Urais. Tufafanue ilani yetu tuliyotekeleza na kilichobaki na kuhamasisha wanachi kupiga kura,” amesema Ally.

Akitoa agizo hilo, amemtaka Mbunge Mteule wa Mtama, Nape Nnauye aliyepo Ilemela, Mwanza kurejea mkoani Lindi kumuandalia mkutano Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete ambaye atakwenda kuzindua kampeni mkoani humo Septemba 8, 2020.

“Tutakuwa wakali kusimamia nidhamu, wagombea wa CCM wapo chini ya kamati za siasa, lazima wafuate maelekezo sio kujiamulia binafsi,” amesisitiza Bashiru Ally.

Wakati mchaka mchaka wa kampeni ikiendelea, NEC imetangaza kuwa wabunge 18 wa chama hicho wamepita bila kupingwa, hivyo wanasubiri kuapishwa ili kutekeleza majukumu yao ya kibunge.

Send this to a friend