Idadi ya wagonjwa wenye maambukizi ya virusi vya corona nchini Tanzania imezidi kupungua ambapo sasa kwa Mkoa wa Dar es Salaam wagonjwa wamebaki wanne tu.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alipokuwa akizungumza katika ziara ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa mkoani Tanga, ambapo ameongeza kuwa mikoa mingine haina wagonjwa kama vile Pwani na Mwanza.
Akitoa mchanganua wa wagonjwa hao waliopo Dar es Salaam amesema kuwa katika Hospitali ya Amana kuna wagonjwa watatu, na mmoja yupo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila.
Akieleza mchakato mzima wa kupambana na virusi hivyo vinavyosababisha homa ya mapafu, Ummy Mwalimu amesema kuwa kilikuwa kipindi kigumu zaidi kwenye uwaziri wake, lakini anamshukuru Mungu kwa namna Tanzania ilivyofanikiwa kukabiliana na virusi hivyo vinavyoendelea kuisumbua dunia.
Kwa upande wake Waziri Kassim Majaliwa amempongeza Ummy Mwalimu kwa namna alivyosimama katika nafasi yake, na kwamba ameonesha kuwa yeye ni mwanamke wa shoka.