Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Seleman Msumi amesema halmashauri imeunda kamati maalum kwa ajili ya kuwafuatilia wagonjwa wenye maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU) ambao wameacha kutumia dawa za kufumbaza virusi hivyo.
Akizungumza katika kikao cha maraza la madiwani amefafanua kuwa, Serikali inatoa dawa za kufubaza virusi hivyo bila gharama yoyote ili ziwasaidie wagonjwa lakini cha kushangaza baadhi yao hawahudhurii kliniki hali inayosababisha afya zao kudhorota.
“Halmashauri tumeunda timu maalum ambayo ina wataalam wa afya na timu hii itashirikiana na wadau kutoka asasi za kiraia zinazojihusisha na sekta ya afya kwa ajili ya kuwatembelea wagonjwa nyumba kwa nyumba kuwapa elimu juu ya umuhimu wa kuhudhuria kliniki na kutumia dawa,” amesema.
Mkurugenzi amebainisha wagonjwa wengine watakofuatiliwa na timu hiyo ni pamoja na wagonjwa wa kisukari na wenye shinikizo la damu ambao wamepangiwa kliniki lakini wanahudhuria kwa kusuasua na wengine wameacha kabisa kutumia dawa bila sababu za msingi.