Mkuu wa Wilaya ya Ilala, amethibitisha kuwa baadhi ya wagonjwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dar es Salaam, Amana, walitaka kutoka warejee majumbani mwao kwa maelezo kuwa hawaumwi.
Akizungumza na Kituo cha Televisheni cha ITV, Sophia Mjema amesema kuwa baadhi ya wagonjwa hao waliofikishwa hospitalini hapo kwa ajili ya uangalizi na matibabu walilazimisha kutaka kutoka, jambo ambalo si utaratibu wa hospitali.
“Sina uhakika kama nivurugu [iliyotokea], lakini wao walikuwa wanalazimisha, wanapiga kelele wanataka kurejea nyumbani,” amesema Mjema akikanusha kuwa kilichotokea ni vurugu kama inavyosemekana.
Kuhusu taarifa kuwa baadhi ya wagonjwa walifanikiwa kutoka, wakatumia usafiri wa mabasi kurejea makwamo, Mjema amesema bado hawana taarifa hiyo lakini kwa sababu hospitalini hapo kuna walinzi, basi watafuatili kujua kama ni kweli wametoka, pamoja na idadi yao na wamekwenda wapi.
Aidha, ameongeza kuwa kwa sababu wagonjwa waliokuwepo wanafahamika pamoja na maeneo walipochukuliwa, hata kama watakuwa wametoroka, basi watapatikana na kurejeshwa, ili wasieneze magonjwa kwa watu wengine.
Amesema kwa sasa hali ni shwari hospitalini hapo, huku akiwataka wananchi kufuata utaratibu kwani endapo watalaamu watathibitisha mtu hana tatizo wao watamruhusu kutoka, na wale waliopo chini ya uangalizi ni lazima waendelee kubaki hospitalini.
Hospitali ya Amana ni moja ya hospitali zilizotengwa kwa ajili ya kupokea watu wenye maambukizi ya virusi vya corona jijini Dar es Salaam.