Wahukumiwa jela miaka 30 kwa kumlawiti mtoto aliyeomba msaada wa hifadhi

0
6

Mahakama ya Kericho nchini Kenya imewahukumu wanaume wawili kifungo cha miaka 30 jela kila mmoja kwa kosa la kumlawiti mvulana wa miaka 16 katika Kaunti ya Kericho mwaka 2023.

Washtakiwa hao, Ezekiel Tanui na Derrick Kipngeno Kirui, wamehukumiwa na Hakimu Mkuu wa Kericho, Fredrick Nyakundi, baada ya kupatikana na hatia ya kutekeleza unyama huo kati ya Oktoba 20 na Novemba 17, 2023, katika kijiji cha Baraka, pembezoni mwa mji wa Kericho.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP), kijana huyo alisafiri kutoka Kipkelion hadi Kericho kuhudhuria sherehe za Mashujaa Day lakini akajikuta hana nauli ya kurudi nyumbani. Hali hiyo ilimlazimu kutafuta msaada, ambapo Tanui alimchukua na kumpa hifadhi katika nyumba yake ya kupangisha.

Hata hivyo, badala ya msaada, kijana huyo alijikuta akifanyiwa ukatili wa kingono na Tanui kwa zaidi ya mwezi mmoja. Baadaye, alikimbilia kwa Kirui akidhani angepata usalama, lakini naye alimfanyia kitendo kama hicho cha unyanyasaji wa kijinsia.

Baada ya kukamatwa, vipimo vya kitabibu vilithibitisha kuwa washitakiwa wote wawili walikuwa na maambukizi ya virusi vya UKIMWI (HIV), lakini mahakama iliwakuta hawana hatia ya kueneza virusi hivyo kwa makusudi baada ya kuthibitika kuwa mwathiriwa alikuwa hana maambukizi.

Mahakama imewapatia adhabu kali ya kifungo cha miaka 30 kila mmoja ili kutoa onyo kali dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa watoto.