Waishio milimani Mwanza kuondolewa kupisha mwekezaji kutoka Brazil
Wakazi waishio maeneo ya mlimani jijini Mwanza wanatarajiwa kuhamishwa katika maeneo hayo ili kupisha wawekezaji kutoka nchini Brazili ambao wanatarajia kuwekeza kwenye sekta ya miundombinu, viwanda na utalii katika maeneo ya Igogo, Isamilo na Kegeto.
Akizungumza na Nipashe, Meya wa Jiji la Mwanza, Sima Constantine amesema wawekezaji hao kutoka jiji la Rio de Janeiro walifika jijini humo kuangalia fursa za uwekezaji, na mpango wa kuwahamisha katika eneo hilo unalenga kuboresha miundombinu pamoja na kukuza sekta ya utalii utakaogharimu TZS bilioni 150.
Aidha, amebanisha maeneo mengine ambayo wawekezaji wanayalenga ni pamoja na ujenzi wa kiwanda cha pembejeo za kilimo kwa ajili ya kuwahudumia wananchi wa kanda ya ziwa, ujenzi wa barabara pamoja na nyumba za ghorofa katika milima mbalimbali inayoangalia Ziwa Victoria.
Costantine ameeleza kuwa jiji limepewa jukumu la kulipa fidia katika maeneo ya Igogo, Isamilo na Kegoto ili kupisha uwekezaji huo.
Pia, wawekezaji hao wamekubaliana na jiji kutafuta ardhi na kukamilisha mipango ya ardhi ndani ya miezi mitatu kuanzia mwanzoni mwa mwezi huu kabla kazi hiyo kuanza.