Waitara afichua siri ya wabunge wengi wa CHADEMA kuhama chama hicho

0
47

Mbunge wa Ukonga kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) amesema kuwa ongezeko la wimbi la wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kukihama chama hicho kunachochewa sana na uongozi mbovu wa chama.

Mwita Waitara ambaye pia ni Naibu Waziri wa TAMISEMI amefafanua kuwa kwa muda wote aliokuwa CHADEMA, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe amekuwa akitumia vibaya fedha za chama, hivyo kukisababishia kuwa kwenye madeni makubwa.

Akitolea mfano mwaka 2014 amesema kuwa “Mbowe alileta kampuni kutoka Marekani iliyolipwa TZS 500 milioni ili iandae ‘fund raise’ kusaidia kwenye uchaguzi mkuu 2015. Lakini hakuna anayejua kampuni hiyo ilikusanya kiasi gani, ziliwekwa wapi, na zilimsaidia mgombea gani.”

Baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 wakiwa kwenye kikao cha chama Mwanza ameeleza kuwa Mbowe alisema ameikopesha CHADEMA TZS 2 bilioni, lakini hakuwa na hana ushahidi wa mkopo huo, na tayari alikuwa amewapanga wajumbe wa kamati kuu kwa kuwapa posho, hivyo walijadiliana deni likashuka hadi TZS 700 milioni, akaingia mkataba na CHADEMA ambapo kila mwezi analipwa TZS 50M kutoka kwenye ruzuku.

Aidha amesema kuwa inakuwa vigumu kwa waliopo ndani ya chama hicho kuzungumza kwa sababu wanahofu watashughulikiwa.

“Watu wanauliza mbona mkitoka CHADEMA ndio mnasema, ukisema ukiwa ndani unashughulikiwa, kwa sababu mwenye chama ni Mbowe na ndiye mwenye maamuzi ya mwisho. Ndio maana Zitto Kabwe alitaka uenyekiti aliwashwa, Kitila Mkumbo na Chacha Wangwe wote wamewashwa,” amesema Waitara.

Ameeleza kuwa haya na mambo mengine mengi ndio yamechangia wabunge na madiwani wengi kukihama chama hicho kwa sababu wanaminywa kutoa fedha, wanakitumika kwa nguvu zao zote, lakini wanaona anayefaidika zaidi ni mtu mmoja.

Amesema yote aliyoyaeleza waliowahi kuwa makatibu wakuu wa chama hicho, Dkt. Wilbrod Slaa na Dkt. Vicent Mashinji wanafahamu hata wakiulizwa watathibitisha.

Julai 2018 Waitara alihama CHADEMA na kujiunga CCM, ambapo aligombea tena ubunge katika jimbo alilokuwa akiliongoza na kushinda.

Send this to a friend