Wajane waomba msaada kupambana na afya ya akili

0
54

Wajane nchini wameiomba Serikali kuwapatia msaada wa kisheria ili kupata haki zao na kusaidiwa huduma ya afya ya akili ili kudhibiti msongo wa mawazo.

Ameyasema hayo Katibu wa Wajane Taifa, Sabrina Tenganamba alipokuwa akiwasilisha risala mbele ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Wajane Duniani yaliyofanyika hapo jana juni 23, 2023 jijini Mbeya.

Akieleza changamoto wanazokabiliana nazo, amesema wajane wengi husingiziwa kuwauwa waume zao na kunyang’anywa haki zao za mirathi, hivyo kupelekea umaskini mkubwa na kupata msongo wa mawazo na wengine kufikia hatua ya kujiua.

“Lakini pia tunaomba wakala wa usajili, ufilisi na udhamini (RITA) ahakiki kumbukumbu za ndoa kwani changamoto nyingine zinaletwa na wanaume kuwa na ndoa zaidi ya moja zilizosajiliwa hivyo kuleta shida wakati wa mirathi”. amesema Sabrina.

Aidha, Wajane wameomba waunganishwe na mifumo ya benki ili wanufaike na fursa za kiuchumi na kufanya uzalishaji.

Akijibu changamoto hizo Dkt. Gwajima amesema Serikali itaimarisha zaidi uratibu wa masuala ya wajane na kusimamia sheria ya msaada wa kisheria Na. 1 ya mwaka 2017 ili kuhakikisha wajane wanapata haki zao.

Pamoja na hayo ameelekeza uandaliwe mkutano wa Chama cha Wajane na watendaji wote kupitia mtandao wa kidigitali ili kujadili changamoto zote na kuzitafutia suluhisho mapema Julai mwaka huu.

Send this to a friend