Wajasiriamali wamshukuru Rais Samia kuwawezesha kushiriki maonesho Sudan Kusini

0
18

Wajasiriamali kutoka maeneo mbalimbali nchini Tanzania wameishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu kwa kuwawezesha kushiriki maonesho ya 24 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki maarufu Nguvu Kazi au Jua Kali yanayofanyika Juba, Sudan ya Kusini.

Wakizungumza Wajasiriamali hao kwa nyakati tofauti wamesema uratibu uliofanywa na Serikali kugharamia usafiri wao na mizigo, hali hiyo imewapa chachu ya kushiri kwa wingi katika maonesho hayo.

Vile vile, Wajasiriamali hao wametumia fursa hiyo kuhamasisha wananchi wa Sudan ya kusini pamoja na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutembelea banda la Tanzania ili kujionea bidhaa bora zinazozalishwa na Watanzania.

“Sisi wajasiriamali tunafarijika sana na tunamshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kutuwezesha kufika Sudan ya kusini ili tuweze kutangaza biashara zetu katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki,” amesema mmoja wa wajasiriamali hao, Janeth Makundi.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Ajira na Ukuzaji Ujuzi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Amos Nyandwi amesema Serikali imeendelea kuratibu ushiriki wa Wajasiriamali Wadogo na wa Kati katika maonesho hayo ili waweze kutangaza biashara zao nje ya mipaka ya Tanzania.

Maonesho ya 24 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki maarufu Nguvu Kazi au Jua Kali yamefunguliwa rasmi na Makamu wa Rais wa Pili wa Sudan ya Kusini, Dkt. James Wani Igga ambapo maonesho hayo yamevutia Wajasiriamali zaidi ya 1,700 kutoka nchi zote Nane (8) wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kushiriki.

Send this to a friend