
Jeshi la Polisi mkoani Dodoma linamshikilia mwanaume mwenye umri wa miaka 33, mkazi wa Mailimbili, kwa tuhuma za kumbaka mwanafunzi wa kidato cha nne mwenye umri wa miaka 19 kwa nyakati tofauti, huku mtuhumiwa mwingine akiendelea kutafutwa.
Taarifa ya Polisi imeeleza kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa mhanga amekuwa akifanyiwa ukatili huo na wajomba zake wawili waliotumia uhusiano wao wa kifamilia kutimiza matamanio yao ya kimwili, wakimtishia kumjeruhi endapo angemueleza mtu yeyote.
“Mara baada ya kupata taarifa kuhusu tukio hilo, Jeshi la Polisi lilianza ufuatiliaji na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja aliyekuwa akijaribu kutoroka, huku juhudi za kumtafuta mtuhumiwa wa pili zikiendelea. Mtuhumiwa aliyekamatwa atafikishwa mahakamani mara uchunguzi utakapokamilika,” imeeleza taarifa hiyo.
Aidha, Jeshi la Polisi limewataka wananchi kuacha kufumbia macho vitendo vya ukatili wa kijinsia na kuacha kufanya usuluhishi wa kesi hizo majumbani, badala yake watoe taarifa kwa vyombo vya dola ili hatua za kisheria zichukuliwe.







