Wajue Marais wa Afrika waliopinduliwa na jeshi wakiwa madarakani

0
54

Mapinduzi ya kijeshi hutokea pale ambapo jeshi au kikundi cha kijeshi kinapochukua udhibiti wa serikali kwa nguvu na kumpindua Rais au kiongozi aliyeko madarakani.

Uongozi mbaya, ufisadi na ukosefu wa ajira vinatajwa kuwa sababu zinazochochea mapinduzi katika nchi husika.

Hawa ni baadhi ya Marais waliopinduliwa na jeshi katika miaka ya hivi karibuni wakiwa madarakani;

Mamadou Tandja – Niger (2010): Mamadou aliondolewa madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi yaliyotokea mnamo Februari 18, 2010 kwa kujaribu kubadili katiba ili kuondoa ukomo wa mihula ya Urais. Alikuwa Rais wa Niger tangu mwaka 1999.

Hosni Mubarak – Misri (2011): Mubarak alikuwa Rais wa Misri kuanzia mwaka 1981 hadi 2011. Maandamano ya raia yalizuka mnamo Januari 2011 yakidai demokrasia, uhuru wa kisiasa, na haki za binadamu. Hatimaye, jeshi lilimuondoa madarakani mwezi Februari 2011 baada ya maandamano makubwa kufanyika.

Muammar Gaddafi – Libya (2011): Gaddafi alikuwa kiongozi wa muda mrefu wa Libya. Maandamano ya awali yaliyofuatiwa na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yalipelekea kuingilia kati kwa jumuiya ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na jeshi la NATO, ambalo lilimsaidia mpinzani wa Gaddafi. Hii ilisababisha kifo cha Gaddafi na kuanguka kwa utawala wake.

Amadou Toumani Touré – Mali (2012): Touré alikuwa Rais wa Mali kwa awamu mbili akihudumu kidemokrasia. Hata hivyo, alikosolewa kwa kukabiliwa na waasi wa Tuareg katika eneo la Kaskazini mwa Mali. Jeshi lilitumia sababu hii kumtoa madarakani mnamo mwaka 2012.

Mohamed Morsi – Misri (2013): Morsi alikuwa Rais wa kwanza wa Misri aliyechaguliwa kidemokrasia baada ya kuondolewa kwa Mubarak. Aliondolewa na jeshi mwaka 2013 baada ya maandamano makubwa ya kupinga uongozi wake.

Blaise Compaoré – Burkina Faso (2014): Compaoré alitawala Burkina Faso kwa miongo mingi baada ya kupindua serikali ya awali. Wananchi walipinga jaribio lake la kubadilisha katiba ili kusalia madarakani, na maandamano makubwa yaliyosababisha kifo cha waandamanaji yalisababisha jeshi kuchukua udhibiti na kumpindua.

Robert Mugabe – Zimbabwe (2017): Mugabe alitawala Zimbabwe tangu uhuru wake, na utawala wake ulikumbwa na migogoro ya kisiasa, uchumi dhaifu na rushwa. Jeshi lilichukua udhibiti wa mji mkuu Harare, na Mugabe alilazimika kujiuzulu baada ya shinikizo la jeshi na maandamano ya umma.

Omar al-Bashir – Sudan (2019): Al-Bashir alitawala Sudan kwa miongo kadhaa, lakini utawala wake ulikumbwa na migogoro ya kisiasa na kiuchumi. Maandamano ya umma yalizidi kuongezeka na hatimaye jeshi liliamua kumpindua na kuchukua madaraka.

Bah Ndaw- Mali (2021): Rais na Waziri mkuu waliondolewa madarakani na Afisa wa jeshi, Kanali Assimi Goïta aliyeteuliwa kuwa Makamu wa Rais katika Serikali ya Mpito baada ya kuondolewa kwa Rais Ibrahim Boubacar Keita mnamo Agosti 2020. Goïta alidai Rais Bah Ndaw na waziri mkuu, walishindwa kutekeleza majukumu yao na walikuwa na njama ya kuhujumu mchakato wa mpito nchini humo.

Roch Kaboré – Burkina Faso (2022): Kuondolewa kwa Kabore kulichochewa na hali ya kutoridhika miongoni mwa vikosi vya usalama kwa madai ya kutoungwa mkono kikamilifu dhidi ya wanamgambo wanaohusishwa na al-Qaeda na kundi la Islamic State.

Mohamed Bazoum – Niger (2023): Wanajeshi wa Niger wakiongozwa na Kanali Amadou Abdramane walitangaza kumuondoa madarakani Rais Bazoum saa chache baada ya rais huyo kushikiliwa katika ikulu ya rais. Sababu za kupinduliwa kwake zimetajwa kuwa ni kutokana na kuzorota kwa hali ya usalama na utawala mbovu.

Ali Bongo – Gabon (2023) Wanajeshi wa Gabon wamejitokeza kwenye televisheni ya Taifa na kutangaza kutwaa mamlaka ya nchi hiyo huku wakibatilisha matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi Rais Ali Bongo ambaye familia yake imetawala nchi hiyo kwa miaka 53. Sababu za kuondolewa kwa Rais Bongo zimetajwa kuwa ni uchaguzi uliojaa udanganyifu na uliopata ukosoaji mkubwa.