Wajue Marais wa Marekani waliowahi kuitembelea Tanzania kikazi

0
72

Tanzania inajiandaa kupokea ugeni mkubwa wa Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris ambaye anatarajiwa kuwasili nchini Machi 29 katika ziara ya kikazi itakayomalizika Machi 31 mwaka huu.

Hii si mara ya kwanza kwa Tanzania kupata ugeni wa kiongozi wa juu Taifa hilo, kwani itakumbukwa kuwa baadhi ya Marais wamewahi kuzuru Tanzania kwa nyakati tofauti.

Hawa ni Marais wa Marekani waliowahi kutembelea Tanzania;

Bill Clinton, 2000
Ndiye alikuwa Rais wa kwanza wa Marekani kukanyaga Tanzania Agosti 28-29, 2000 na kupokelewa na Rais wa awamu ya tatu, Hayati Benjamin Mkapa.

Alifika mkoani Arusha baada ya kupewa mwaliko na Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Hayati Nelson Mandela ili kuweka uzito katika juhudi zake za kuleta amani nchini Burundi.
Ujio wake ulilenga kushuhudia pia utiaji saini makubaliano yenye lengo la kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka saba nchini Burundi.

George Bush, 2008
Alifika nchini Februari 16-19, 2008 wakati wa awamu ya nne ya Rais Jakaya Mrisho Kikwete ikiwa ni katika ziara ya mataifa matano barani Afrika; Tanzania, Rwanda, Benin, Ghana na Liberia kwa ajili ya mazungumzo na wakuu wao wa nchi na kutembelea miradi inayofadhiliwa na serikali ya Marekani.

Bush aliangazia juhudi za kuboresha afya barani Afrika katika kukabiliana na VVU/UKIMWI na mpango wa kutokomeza Malaria.

Barack Obama, 2013
Aliwasili nchini Julai 1, 2013 akitokea Afrika Kusini na kupokelewa na aliyekuwa Rais wa awamu ya nne, Jakaya Mrisho Kikwete na mkewe, Salma Kikwete katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.

Katika ziara yake barani Afrika iliyoanzia nchini Senegal, Afrika kusini na kisha Tanzania, aliongozana na wajumbe 700, wengi wao wakiwa wafanyabiashara waliokuja kuona fursa za uwekezaji katika maeneo mbalimbali nchini.

Moja ya mipango ya ziara hiyo ilikuwa ni kutembelea kituo cha umeme cha Ubungo, ukiwa ni mpango wa miaka mitano wa dola za Marekani bilioni saba ili kusaidia mradi wa umeme barani Afrika kwa kushirikiana na sekta binafsi.

Ziara ya Kamala nchini inagusia maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na athari za vita vya Urusi na Ukraine, usalama wa chakula, ukuaji wa demokrasia na fursa za kibiashara na uwekezaji.