Polisi mkoani Morogoro wanawashikilia watu wawili , Paulo Erick (48) maarufu Shayo na Dickson Mashamu (35) maarufu kwa jina la Tajiri Masu au Papaa, kwa tuhuma za udanganyifu na wizi wa kutumia madawa.
Kamanda wa Polisi mkoani humo, Fortunatus Musilimu amesema Erick alikuwa akiendesha magari ya kifahari, aliwapeleka wanawake katika hoteli za kifahari na kuwapa kitambaa cha kufuta jasho (leso) na walipokitumia walipoteza fahamu na kuwaibia simu, fedha na vitu vya thamani.
Aidha mtuhumiwa mwingine, Mashamu mkazi wa Buza Tanesco, Dar es Salaam alikamatwa Agosti 27, mwaka huu akitokea jijini Dar es Salaam ambapo anadaiwa kuwaibia wanawake akijifanya ni mtumishi wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) makao makuu Dodoma.
Ameongeza kuwa mtuhumiwa alikuwa akinunua mvinyo (red wine) au supu na kuweka dawa ili mtumiaji apoteze fahamu, na baada ya kuwalewesha aliwalazimisha wataje namba za siri za kadi za benki na kisha kuwaibia fedha.
Kamanda Musilimu ameeleza kuwa mtuhumiwa alikuwa akivaa mavazi nadhifu na kuwalenga wanawake wenye uwezo wa kiuchumi, pia alikuwa akisakwa kwa kufanya matukio kwenye Mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza na Arusha akituhumiwa pia kwa ulawiti na ubakaji kwa wanawake.