Wakamatwa kwa wizi wa mafuta ya magari yanayotumika katika ujenzi wa barabara

0
79

Jeshi la Polisi mkoani Kigoma linawashikilia watu watano kwa tuhuma za kuiba mafuta ya dizeli lita 700 kutoka katika mitambo na magari yanayotumika kujenga barabara ya Kasulu – Manyovu, mkoani humo.

Akizungumza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Filemon Makungu amethibitika kukamatwa kwa watu hao ambapo amesema Agosti 25 mwaka huu katika eneo la Murubona Kasulu, Polisi walifanikiwa kukamata mafuta hayo wakiwa katika doria.

‘’Tarehe 25 Agosti katika kijiji cha Ruhita wilayani Kasulu Kigoma, Askari wakiwa katika doria waliwakamata watuhumiwa hao watano ambao ni George Antony (42), Athuman Ramandhan (36), Anderson Antony (45), Mpaji Firishi (30) na Fred Kachelelo (38),” amethibitisha Kamanda Makungu.

Ameongeza kuwa watuhumiwa wote wamekamatwa wakiwa na mafuta lita 700 zikiwa kwenye pipa 22 na madumu 23, na kwamba baada ya upelelezi kukamilika watuhumiwa watafikishwa Mahakamani.