Walemavu wageuzwa kitega uchumi jijini Dar es Salaam

0
37

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Wenye Ulemavu, Ummy Ndeliananga amekemea vikali vitendo vya udhalilishaji watu wenye ulemavu ikiwemo suala watu ambao wamekuwa wakitumia kundi hilo kujinufaisha.

Amesema kumekuwa na vitendo vya udhalilishaji wa watu wenye ulemavu ambavyo vimekuwa vikiendelea katika jamii na vitendo hivyo vinapelekea ukiukwaji kwa haki zao.

“Watu wenye ulemavu wanahaki zao za msingi na ndio maana Serikali imekuwa ikuchukua hatua mbalimbali kuzuia vitendo vya udhalilishaji kwa kundi hilo na katika kulitambua hilo sheria mbalimbali zimekuwa zikitungwa lengo hasa ni kulinda maslahi na kuboresha maisha ya watu wenye ulemavu,” amesema Ummy

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Wenye Ulemavu, Ummy Nderiananga akimchapa viboko mmoja wa vijana ambao wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya kudhalilisha watu wenye ulemavu kuombaomba mitaani.

Ameongeza kuwa wapo baadhi ya watu ni kama mawakala ambao wanawatoa watu wenye ulemavu katika mikoa mbalimbali na kuwaleta jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuwafanya ombaomba mitaani.

“Inastahajabisha kuona mtu anawachukua watu wenye ulemavu na kuwakodisha viti mwendo (wheelchair) ili wakaombe mtaani huku kila siku anachukua fedha hizo kwa wenye ulemavu lengo ikiwa ni kujinufaisha kwa maslahi binafsi.

Serikali itahakikisha ina shughulikia suala hili la udhalilishaji wa watu wenye ulemavu ili waweze kupata haki zao, sambamba na kuwalindwa na kufanya kundi hilo liheshimike katika jamii,” ameongeza Naibu Waziri Ummy

Aidha, amewataka wananchi kutowaonea aibu wahusika wanaofanya vitendo hivyo badala yake wawe huru kutoa taarifa katika vyombo vya kisheria ili wachukuliwe hatua.

Sambamba na hayo, ametumia fursa hiyo kuwaelimisha watu wenye ulemavu juu ya fursa ya mikopo inayotolewa na serikali kupitia halmashauri (2% Watu wenye Ulemavu) ili waweze kuanzisha shughuli zitakazo wapatia kipato badaya ya kuombaomba mitaani.

Send this to a friend