Walimu wafungiwa ofisini kwa kushindwa kurejesha mikopo

1
28

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Sophia Mjema ametoa maagizo kwa Jeshi la Polisi kufuatilia na kuwachukulia hatua taasisi za mikopo zinazodaiwa kuwashikilia baadhi ya walimu katika vituo vyao vya kazi wanaposhindwa kulipa madeni yao.

Kauli hiyo imefuatiwa baada ya tamko la Mwenyekiti wa Chama cha walimu Tanzania Manispaa ya Shinyanga, Meshack Mashigala kudai kila mwaka kumekuwa na matukio ya baadhi ya walimu kukamatwa na wakopeshaji na kisha kufungiwa katika ofisi zao na kuwadhalilisha mbele ya wanafunzi wanaposhindwa kulipa kwa wakati.

“Walimu wangu wanapokopa tu riba inakuwa asilimia 20, wanakabidhi kadi za benki na kutoa namba za siri za benki, wakati wa marejesho wanakuta riba imepanda hadi asilimia 100, hali ambayo hawezi kulipa na anaanza kuishi kama ndege na shuleni anashindwa kuhudhuria vipindi alivyopangiwa kufundisha,” amesema Mwenyekiti.

Ameendelea kusema baadhi ya walimu wamenyang’anywa kadi zao za benki baada ya kukopa fedha katika taasisi hizo ambazo nyingi hazijasajiliwa, na wapo waliokamatwa kazini na kuwekwa katika mahabusu wanazozimiliki ambazo ni kinyume cha sheria.

Kamanda wa Polisi Mkoani Shinyanga, George Kyando amesema baadhi ya walimu wamekuwa wakifika polisi kuomba barua ili waende benki kuomba kadi nyingine kwa madai kadi ya mwanzo imepotea.

Kyando amewataka walimu wanapohitaji mikopo waende katika taasisi zinazotambulika na Serikali ambako kuna viwango vinavyotakiwa kisheria.

Send this to a friend