Walimu wanaojitolea kupewa kupaumbele ajira 4,000 za Serikali
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Lela Muhamed Mussa amesema walimu wanaofanya kazi kwa kujitolea watapewa kipaumbele katika ajira 4,000 zitakazotolewa na Serikali.
Ameyasema hayo wakati akiwasilisha bajeti ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2022/2023 katika Baraza la Wawakilishi mjini Unguja.
Waziri ameeleza kuwa, wizara inafanya mchanganuo wa mahitaji na imeweka kipaumbele cha walimu wa masomo ya kemia, fizikia, baiolojia na hisabati kwa kuwa uhitaji wao ni mkubwa zaidi.
Aidha, amebainisha kuwa maeneo yaliyopewa kipaumbele zaidi katika ajira hizo ni Tumbatu, Uzi, Njau na Ngambwa kilichopo Unguja na kuahidi kuwa wizara itatumia fedha za UVIKO-19 zilizotengwa kwa ajili ya miradi yote muhimu.
“Serikali ya Zanzibar imetenga shilingi bilioni 68,500 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ikiwemo ujenzi wa shule za ghorofa kuanzia msingi hadi sekondari pamoja na nyumba za walimu katika visiwa vidogo,” amesema.