Walimu wawageuza wanafunzi wapenzi wao, wazazi waangua kilio

0
62

Baadhi ya waalimu wilayani Kaliua mkoa wa Tabora wamelalamikiwa na wazazi pamoja na walezi wilayani humo kwa kuwalaghai wanafunzi na kufanya nao mapenzi kisha kuwapa ujauzito.

Malalamiko hayo yametolewa mbele ya Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Itikadi na Uenezi, Shaka Hamidu katika ziara yake mkoani humo.

Akizungumza Nixon Erasto (50) amedai baadhi ya waalimu wa Shule ya Sekondari Mwongozo hufanya mapenzi na wanafunzi hadi kuwapa ujauzito pasipo kuchukuliwa hatua yoyote.

“Kuna mwalimu kakamatwa kwa kufanya mapenzi na mwanafunzi lakini akatoroka na hajakamatwa hadi leo, na sio huyo peke yake, kuna walimu wengi wenye tabia za namna hiyo, kiongozi tunaomba utusaidie,” amesema.

Akijibu malalamiko hayo, Mkuu wa Wilaya hiyo, Paul Matiko Chacha amekiri kuwepo kwa baadhi ya walimu wenye tabia za namna hiyo, na kwamba tayari hatua stahiki kwa baadhi ya walimu hao zimechukuliwa.

Hata hivyo Shaka amemwagiza Mkuu wa Wilaya kuwasaka walimu wanaolalamikiwa kujihusisha na vitendo hivyo, na kuhakikisha wanachukuliwa hatua kali za kinidhamu ili kukomesha tabia za namna hiyo.

Send this to a friend