Serikali imesema ili kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) shuleni, ina mpango wa kugawa vishkwambi vilivyotumika katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi kwa walimu wote nchini ili kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Juma Kipanga alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (CHADEMA), Subira Mwaifunga aliyehoji mpango wa Serikali kueneza TEHAMA katika kufundisha ili kuwaokoa walimu dhidi ya matatizo ya mgongo na shingo.
Naibu Waziri ameongeza kuwa vishkwambi vilivyotumika katika zoezi la Sensa ni zaidi ya laki mbili na elfu tano, Serikali kupitia Wizara ya Elimu imeongeza vishkwambi vingine zaidi ya laki moja hivyo idadi ya vishkwambi vilivyonunuliwa vitatosheleza walimu wote.
Aidha, amesema kwa wanafunzi wenye matatizo ya kuona na ulemavu, Serikali inaendelea na jitihada za kuhakikisha wanapata vifaa vya kujifunzia na kufundishia somo hilo, pamoja na kuimarisha vituo vya kufundishia walimu.
Ameongeza, “ Serikali iko katika mpango wa kuandaa maktaba mtandao ambao utakapokamilika vitabu vyote vya ziada na kiada vitakuwepo kwenye maktaba hiyo, na itakuwa rahisi kwa walimu na wanafunzi kupata mafunzo na kupata mada mbalimbali kutoka kwenye maktaba hizo.”