Waliochangia bilioni 7 za Royal Tour kutajwa

0
43

Rais Samia Suluhu Hassan amesema wakati wa uzinduzi wa filamu ya Tanzania: The Royal Tour jijini Dar es Salaam Mei 8 mwaka huu watawataja watu/taasisi zote zilizochangia fedha iliyotumia kutayarisha filamu hiyo inayoangazia fursa za utalii na uwekezaji nchini.

Akifanya mahojiano na Azam TV, Rais amesema katika uzinduzi wa Arusha waliwashukuru watu hao kwa ujumla, lakini Dar es Salaam watamtaja mmoja mmoja.

“Zile bilioni 7 sikuchukua serikalini, nilichangisha kwa wafanyabiashara ambapo watafaidika na yatakayotokana na ile filamu… Tutakapokuwa Dar es Salaam tutamtaja kila mmoja aliyechangia,” amesema.

Aidha, amesema kiwango hicho cha fedha kinaweza kuonekana na kikubwa,  lakini kuzingatia ubora wa filamu hiyo yenye viwango vya Hollywood, na matokeo yake itakayoleta kwenye utalii, biashara na uwekezaji, yatakuwa ni makubwa huku akisisitiza kwamba “ninajua nilichokifanya.”

Katika muktadha huo amewajibu wale wanaosema kwamba ana safiri sana nje ya nchi, akiwataka kuangalia matokeo ya ziara zake, na kuangalia hali ya kibiashara ilivyokuwa Tanzania wakati ambao hatukuwa tukisafiri na sasa ambapo tunasafiri.

Ametolea mfano wa  nchi chache alizokwenda kama Kenya ambako alitatua vikwazo vya kibiashara, Uganda alikamilisha taratibu za  kuanza ujenzi wa bomba la mafuta, Umoja wa Ulaya, Dubai, Marekani ambako ameitangaza Tanzania na kusaini hati za mashirikiano na mikataba ya uwekezaji itakayowanufaisha Watanzania.

Send this to a friend