Waliofanya uzembe ghorofa lililoanguka Magogoni kuchukuliwa hatua

0
31

Kufuatia kuanguka kwa jengo la ghorofa mbili katika eneo la Magogoni, Dar es Salaam, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amezielekeza Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), Bodi ya Usajili wa Wakandarasi (CRB) na Bodi ya Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB) kufika mara moja eneo la tukio na kushirikiana na timu za wataalamu kutoka mamlaka nyingine za Serikali kujua sababu ya kuanguka kwa jengo hilo.

Bashungwa amezielekeza bodi hizo kuchukua hatua stahiki kwa wote ambao wamekiuka sheria za kitaaluma katika ujenzi na usimamizi wa jengo hilo.

Aidha, amezitaka bodi hizo kuhakikisha wanaendelea kusimamia miradi ya ujenzi ikiwemo barabara, madaraja na majengo, na kuhakikisha wajenzi na wasimamizi wa miradi hiyo wanafanya kazi kwa kuzingatia miiko na maadili ya taaluma zao.

Mbali na hayo, waziri amewapa pole majeruhi na familia iliyompoteza mpendwa wao huku akisisitiza wakandarasi, wahandisi na wamiliki wa majengo kuhakikisha wanatumia wataalamu waliosajiliwa ili kuepusha kutokea kwa madhara yanayoweza kusababisha majeruhi na vifo.

Send this to a friend