Idadi ya watu waliofariki kwenye ajali iliyohusisha lori na magari mengine madogo matatu katika eneo la Ngaramtoni Kibaoni mkoani Arusha imefikia 25 na wengine 21 wakijeruhiwa
Akitoa taarifa ya ajali hiyo Kamishna wa Polisi Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, CP Awadhi Juma Haji alipofika katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Arusha Mount Meru, amesema ajali hiyo ilitokea Februari 24,2024 saa 11 jioni katika Barabara ya Arusha Namanga ambapo ilihusisha lori lenye namba za usajili KAC 943 H aina ya Mack lenye tela namba za usajili ZF 6778 mali ya kampuni ya KAY Construction ya Nairobi Nchini Kenya.
CP Awadhi ametaja idadi ya waliofariki katika ajali hiyo kuwa ni wanaume 14 wanawake 10 na mtoto mmoja wa kike ambao jumla yao ni 25 huku akiitaja idadi ya raia wa kigeni waliofariki kuwa ni saba.
Aidha, amesema chanzo cha ajali hiyo ni kufeli breki ya lori kitendo kilichopelekea lori hilo kuyagonga magari mengine yaliyokuwa mbele yake huku akibainisha kuwa Jeshi hilo linaendelea kumtafuta dereva aliyesababisha ajali hiyo ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake.