Waliopata msamaha wa Rais kufuatiliwa

0
40

Zikiwa ni siku chache tangu Rais Samia Suluhu Hassan kutoa msamaha wa vifungo kwa wafungwa 3,826, Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP) Simon Sirro amewaagiza makamanda wa jeshi hilo kuwa na ripoti itakayo wawezesha kuwafatilia wafungwa hao kwa ukaribu ili kujua mienendo yao uraiani.

Akizungumza jana katika maadhimisho ya miaka 58 ya Muungano jijini Arusha, IGP amewataka wafungwa hao kufuata sheria, kanuni na taratibu za nchi kwa kutojihusisha tena na vitendo vya kiuhalifu.

“Nitoe angalizo na onyo kwa wale wanaotoka gerezani, mnapotoka wananchi wanawaangalia mnafanya nini, na mnaporudia makosa mnakuwa ni kero kwa watanzania na wakishawachoka mwisho wa siku wanaamua kuchukua sheria mkononi.”amesema IGP Sirro.

Aidha alitoa angalizo kwa wazazi wasilalamike pale watoto au familia zao zitakaporudishwa gerezani kwa kusumbua watu, hivyo Jeshi la polisi halitakuwa na muhali na mtu wa namna hiyo na kuahidi kuwashughulikia.

Send this to a friend