Wambura atuma salama kwa wahalifu

0
15

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, DCI Camilius Wambura amesema Jeshi la Polisi halitamvumilia mtu yeyote atakayeendelea kujihusisha na vitendo vya uhalifu hususani wakati huu ambao jeshi hilo linaendelea na operesheni kali ya kupambana na vitendo hivyo.

DCI Wambura ameyasema hayo leo jijini Dodoma katika kikao kazi kilichowashirikisha Maofisa wa Makao Makuu ya Upelelezi na Wakuu wa Upelelezi wa mikoa nchini kwa lengo la kupanga mikakati ya kupambana na uhalifu pamoja na kutathmini hali ya uhalifu nchini.

“ Wito wangu kwa wahalifu ni bora watafute kazi nyingine ya kufanya kwa kuwa hatuna huruma kwa watu hao na wananchi waendelee kutupatia taarifa zao ili tuhakikishe nchi yetu inaendelea kuwa salama,“ amesema Wambura.

Kwa upande wake Naibu DCI, DCP Faustine Shilogile amesema wanaendelea kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa takwimu na utoaji wa mafunzo kwa watendaji wa idara hiyo ili kuwa na wapelelezi wenye weledi ambao watasaidia kuharakisha upelelezi wa kesi zinazoripotiwa katika vituo vya polisi.

Katika kikao hicho, Wakuu wa Vitengo kutoka Idara ya Upelelezi wa Makao Makuu ya Polisi walipata fursa ya kutoa elimu kwa wakuu hao wa upelelezi wa mikoa jinsi vitengo vyao vinavyofanya kazi pamoja na Mwakilishi wa Ofisi ya Mwendesha Mashtaka.

Send this to a friend