Wamiliki wa maghala waihakikishia Serikali kuna mafuta ya kutosha nchini

0
61

Kutokana na taarifa zilizosambaa kuhusu uhaba wa mafuta nchini, Wamiliki wa maghala ya mafuta wameihakikishia Serikali uwepo wa mafuta ya kutosha kwa upande wa petroli na dizeli huku wakiahidi kutoa ushirikiano katika usambaji wa mafuta kwenye maeneo mbalimbali yenye uhitaji.

Hayo yameelezwa katika ziara ya Waziri wa Nishati, January Makamba aliyeambatana Kamishna wa Mafuta na Gesi Asilia, Michael Mjinja na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Dkt. James Andilile wakati wa akikagua zoezi zima la upokeaji na usambazaji wa mafuta nchini.

Akijibu swali la Waziri wa Nishati, January Makamba kuhusu tetesi za ukosefu wa mafuta nchini, Mkurugenzi Mkuu Mount Meru, Charles Maingu amewahakikishia uwepo wa mafuta ya kutosha, akibainisha kuwa ndani ya siku 10 zilizopita wametoa mzigo wa mafuta wa lita milioni 28 yaliyosafirishwa ndani ya nchi na nje ya nchi, na pia Agosti mwaka huu watapokea mzigo mwingine wa dizeli milioni 27 na petroli lita milioni 40.

Mkurugenzi Mtendaji Puma Energy, Fatma Abdallah amesema Julai mwaka huu kumekuwa na mahitaji makubwa ya mafuta, akisema tayari wameuza petroli na dizeli lita zaidi ya milioni 36 ikilinganishwa na mwaka 2022 ambapo waliuza milioni 30 pekee.

Waziri Mkuu atoa siku saba TARURA, DAWASA kukamillisha barabara ya Muhimbili

“Napenda niwahakikishie mafuta yapo ya kutosha. Tuna dizeli zaidi ya lita milioni 12 kwenye matenki, tuna petroli zaidi milioni 5 kwenye matenki lakini bado tunaendelea kupokea, tuna mzigo wa lita milioni 80 ambao tunategemea kuupokea kuanzia wiki ijayo mpaka Agosti 23,” amesema Fatma.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Bandari, Mrisho Mrisho amesema shughuli ya kushusha mafuta bandarini inafanyika kila siku huku akiwatoa hofu Watanzania kuhusu upatikanaji wa nishati hiyo.

“Katika mipango ya baadaye tunajipanga zaidi kuboresha maeneo mbalimbali ya bandari likiwemo la kupokelea mafuta. Leo ni siku ya tatu meli inashusha kesho inamaliza na kuingia nyingine,” amesema Mrisho.

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati, January Makamba amesema lengo la ziara hiyo ni kujua hali ya mafuta yaliyopo katika maghala ya wafanyabiashara hao, sambamba na kusikia changamoto zinazowakabili wadau hao wa sekta hiyo.

Send this to a friend