Wanachama 11 wa CHADEMA wakamatwa kwa kufanya mkusanyiko usio halali

Jeshi la Polisi mkoani Rukwa limewakamata wanachama 11 wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kati yao wakiwemo viongozi wanne wa chama hicho kwa kufanya mkusanyiko usio halali.
Taarifa ya Polisi imesema viongozi hao ni Katibu mwenezi wa Baraza la Vijana CHADEMA Jimbo la Nkasi Kaskazi, Winfrida, Khenani, Katibu wa CHADEMA Jimbo Nkasi Kaskazini, Godfrid Bendera, Katibu Baraza la Wazee CHADEMA Wilaya ya Nkasi, Evarist Mwanisawa na Mwenyekiti CHADEMA Kata ya Majengo, Scolastica Mwalonde.
Aidha, Jeshi la Polisi limewataka Aida Khenani, Mbunge wa Jimbo la Nkasi Kaskazini na Albeto Kaliko, aliyekuwa Diwani wa kata ya Ilete kujisalimisha Polisi au Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai mkoani humo kwa kupanga mkusanyiko usio halali.
“Kufuatia kukamatwa kwa wanachama hao wa CHADEMA, kumeibuka watu wanaotuma taarifa za uongo, upotoshaji na za kubuni kwenye mitandao ya kijamii wakiwa na lengo la kuitia hofu jamij ya Watanzania au kulichonganisha Jeshi la Polisi kwa wananchi.
Hivyo Jeshi la Polisi linamtaka mtu mmoja aitwaye Alfred Sotoka kuripoti Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Rukwa kufuatia kutuma taarifa za uongo kwenye mitandao ya kijamii kuhusiana na tukio hii. Asijifiche kwani atasakwa popote alipo,” imesema.
Jeshi la Polisi limewaomba wananchi kufuata sheria wanapotaka kufanya mkusanyiko.








