Wanachama 374 wajiondoa CUF, wamtupia lawama Lipumba

0
24

Wanachama 374 wa Chama cha Wananchi (CUF) wamejivua uanachama wa chama hicho wakidai Mwenyekiti Profesa Ibrahim Lipumba anakwenda kinyume na katiba ya chama hicho.

Katika taarifa iliyosomwa na Katibu wa Kamati ya Maazimio CUF, Shahada Issa imedai chama hicho kupitia Mwenyekiti Profesa Lipumba kimekuwa na utaratibu wa wa kuwafukuza viongozi wenye uwezo wa kukipambania chama na kuwaacha viongozi mizigo ambao hawajui historia ya CUF.

“Maamuzi ya CUF yamekuwa yakifanywa na mtu mmoja ambaye ni Lipumba na sio vikao vya chama, hivyo inapelekea CUF kuwa kampuni binafsi ya mtu na kuacha malengo ya awali ya kuwapigania Watanzania wote kupitia kauli mbiu yake ya haki sawa kwa wote,” imeeleza taarifa ya wanachama.

TBS kukichukulia hatua kiwanda kinachozalisha Safari Premium Tea

Aidha, wanachama hao pia wamedai Baraza Kuu kupitia Profesa Lipumba liliwafukuza wajumbe saba wa chama hicho pamoja na kuondoa Kamati Tendaji Wilaya ya Kinondoni kinyume na katiba ya chama, ambapo wamedai katiba ya chama toleo la 2014 inasema ni Kamati Tendaji Taifa pekee ndiyo yenye mamlaka ya kuvunja kamati tendaji za Wilaya kwa mujibu wa katiba ibara ya 85 kifungu kidogo cha 13.

“Sisi kama wanachama tuliokutana hapa leo katika ukumbi wa Garden baada ya kutafakari kwa kina tumeamua kwa pamoja kujivua nafasi zetu kwa wale ambao wana nafasi ndani ya chama na kujiondoa rasmi katika Chama cha Wananchi CUF leo tarehe 23/2/2023, na baada ya tafakari kwa kina tutatoa taarifa rasmi ya wapi tutaelekea,” wamesema.

Send this to a friend