Wanafamilia saba wakamatwa kwa kumchapa viboko ndugu aliyehudhuria maombi

0
78

Polisi wamewakamata watu saba wa familia moja ya dini ya Kiislamu nchini Uganda kufuatia video iliyowaonesha wakimpiga ndugu yao Shakira Naula (18) kwa madai ya kutowatii ndugu zake na kuhudhuria maombi kanisani.

Tukio hilo lilinaswa kwenye video na watu wasiojulikana ambao waliisambaza kwenye mitandao ya kijamii, ikionyesha wanaume wawili wakimkandamiza binti huyo chini huku wanafamilia wengine wakimpiga viboko 100.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Msemaji wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Bukedi, Samuel Semewo amesema mchungaji wa kanisa hilo mwenye umri wa miaka 38 alitoa taarifa ya shambulio hilo katika Kituo cha Polisi cha Kibuku.

“Tulichukua hatua haraka na tukawachukua baadhi ya watu kutoka katika familia moja wilayani Kibuku walioshiriki katika shambulio la kikatili la Shakira Naula mwenye umri wa miaka 18,” msemaji wa polisi, Samuel Semewo ameeleza.

Naula amekuwa akiishi na shangazi yake Musenero Ziyadi baada ya mama yake mzazi kusafiri nchini Saudi Arabia kwa ajili ya kufanya kazi.

Send this to a friend