Wanafunzi 102 wafutiwa matokeo na NECTA

0
55

Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) limetangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha nne uliofanyika Novemba 2023, ambapo jumla ya watahiniwa 484,823 sawa na asilimia 87.65 waliofanya mtihani huo wamefaulu, wasichana wakiwa 257,892 sawa na asilimia 86.17 na wavulana wakiwa 226,931 sawa na asilimia 89.40.

Akitangaza matokeo hayo Katibu Mtendaji wa NECTA, Dkt. Said Mohamed amesema takwimu zinaonesha kuwa kati ya shule zote 5,343 zenye matokeo, shule 5,334 sawa na asilimia 99.83 zimepata wastani wa Daraja A mpaka D huku shule tisa zikipata Daraja la F.

Tazama hapa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2023

Aidha, baraza limefuta matokeo ya watahiniwa 102 wa mtihani wa kidato cha nne ambao wamebainika kufanya udanganyifu wakiwemo wanafunzi watano walioandika matusi kwenye karatasi zao za majibu.

Mbali na hivyo, baraza limezuia kutoa matokeo ya watahiniwa 376 ambao walipata matatizo ya kiafya na kushindwa kufanya mtihani, na kupewa fursa ya kufanya mtihani kwa masomo ambayo hawakuyafanya mwaka huu 2024.

Kwa upande wa ufaulu wa somo la hesabu, NECTA imesema ufaulu umeendelea kuwa chini ya wastani kama ilivyokuwa mwaka 2022. Hata hivyo, imebainisha kuwa ufaulu wake umeendelea kuimarika mwaka huu na kufikia asilimia 25.42 kutoka asilimia 20.08 mwaka 2022.

Send this to a friend