Wanafunzi 30,675 waliopata mikopo awamu ya kwanza

0
43


Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza orodha ya awamu ya kwanza yenye wanafunzi 30,675 wa Mwaka wa Kwanza kwa mwaka wa masomo 2019/2020 waliofanikiwa kupata mikopo yenye thamani ya TZS 113.5 bilioni.

Katika mwaka huu wa masomo, Serikali imetenga TZS 450 bilioni zinazolenga kuwanufaisha jumla ya wanafunzi 128,285. Kati yao, zaidi ya wanafunzi 45,000 ni wa mwaka wa kwanza na wengine 83,285 ni wenye mikopo wanaoendelea na masomo. Mwaka 2018/2019, fedha zilizotengwa na kutolewa zilikua TZS 427.5 bilioni na ziliwanufaisha jumla ya wanafunzi 123,283 wakiwemo 41,285 wa mwaka wa kwanza.

Akizungumza na wanahabari leo (Alhamisi, Oktoba 17, 2019) na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Abdul-Razaq Badru, amesema katika orodha hiyo, wanaume ni 19,632 (64%) na wanawake ni 11,043 (36%).

Badru amefafanua kuwa waombaji mikopo wafunfue akaunti zao binafsi (SIPA – Student’s Individual Permanent Account) walizofungua kuomba mkopo kupitia mfumo wa HESLB (olas.heslb.go.tz) ili kupata taarifa za mikopo.KUONA ORODHA YA AWAMU YA KWANZA, BOFYA HAPA.

                                                            Makundi Maalum – Yatima, Wenye ulemavu n.k

Kuhusu makundi maalum yenye uhitaji, Mkurugenzi Mtendaji huyo amesema katika orodha ya awamu ya kwanza yenye wanafunzi 30,675, wapo wanafunzi 6,142 ambao ni yatima au wamepoteza mzazi mmoja, wenye ulemavu 280 na wengine 277 wanaotoka katika kaya zinazofadhiliwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

“Katika makundi maalum pia tuna wanafunzi 1,890, sawa na asilimia 6 ya wanafunzi 30,675 wa awamu ya kwanza ambao walisoma shule binafsi lakini kutokana na hali duni ya uchumi, walifadhiliwa na walithibitisha kwa kuweka nyaraka sahihi,” amesema Badru.

                                                               Kutangazwa orodha ya awamu ya pili

Kuhusu awamu ya pili, Badru amesema HESLB kabla ya Oktoba 25 ya wiki ijayo baada ya kukamilishwa kwa uchambuzi wa maombi ya mikopo kutoka kwa wanafunzi waliochelewa kukamilisha taratibu za udahili au kuchelewa kurekebisha maombi yao ya mkopo mtandaoni.

                                                                               Wito kwa wanafunzi

Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Uchambuzi na Upangaji Mikopo wa HESLB Dr. Veronica Nyahende amewataka wanafunzi ambao taarifa zao hazijakamilika, kukamilisha ili wenye sifa wapangiwe mkopo.

“Kuna kama wanafunzi 1,000 ambao maombi yao hayajakamilika, watumie muda huu hadi tarehe 19 kukamilisha ili wenye sifa nao tuwapangie mkopo,” amesema.

MWISHO

Send this to a friend