Wanafunzi 47,000 wa mwaka wa kwanza wapewa mikopo

0
16

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetoa orodha ya wanafunzi wa elimu ya juu 47,305 wa mwaka wa kwanza waliopangiwa mikopo yenye thamani ya TZS bilioni 150.03 kwa mwaka wa masomo 2020/2021 ambapo kati ya wanafunzi hao wanaume ni 26,964 sawa na 57.37% na wanawake ni 20,341, sawa na 42.63%.

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru amesema kuwa Serikali imeongeza bajeti ya fedha kwa ajili ya wanafunzi watakaonufaika na mkopo ambapo kwa mwaka huu kiasi kilichotengwa ni TZS bilioni 464 ambapo ni ongezeko la 15% ikilinganishwa na mwaka jana.

Aidha katika mkutano huo Badru amesema wanafunzi wenye mikopo wanaoendelea na masomo katika vyuo mbalimbali nchini wapatao 44, 629 wamepangiwa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 155.06.

Badru amewataka wanafunzi walionufaika na mkopo wa elimu ya juu kuwa waaminifu na kulipa mikopo hiyo kwa wakati ili iweze kuwasaidia wanafunzi wengine wenye uhitaji.

“… mnaokopa mnapaswa kurejesha haraka ili pesa hizo ziweze kusaidia na wadogo zenu na kama mko hapa mchakato wake ni mfupi tu.”