Wanavyuo waliomdhalilisha mwenzao kisa Mwijaku wafikishwa mahakamani

Wanafunzi watatu wanaodaiwa kumdhalilisha mwanafunzi mwenzao wa Chuo Kikuu Ardhi, Magnificat Kimario, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kusomewa mashtaka yanayowakabili.
Wanafunzi hao wamefikishwa mahakamani leo kufuatia tukio la Aprili 20, 2025, ambapo video inayowaonesha wasichana wakigombana, ilisambaa mitandaoni na kuzua mjadala mkubwa, huku jina la mtu anayefahamika kwa jina la Mwemba Burton Mwemba, maarufu kama Mwijaku, likitajwa.
Taarifa iliyotolewa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, imesema kwa mujibu wa taarifa rasmi ya Jeshi la Polisi iliyotolewa Aprili 24, 2025, watuhumiwa hao wametiwa nguvuni na kuhojiwa kuhusiana na tukio hilo.
“Wanafunzi waliotajwa katika taarifa hiyo ni: 1-Mary Matogoro, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wa pili ni Ryner Mkwawili, mwanafunzi wa Chuo Kikuu Ardhi n awa tatu ni Asha Juma, mwanafunzi wa Chuo cha Uhasibu, Dar es Salaam (TIA),” imesema taarifa hiyo.
Aidha, imesema Jeshi la Polisi limethibitisha kuwa limemuhoji pia Mwemba Burton Mwemba maarufu kama Mwijaku kuhusiana na tuhuma hizo, “ingawa haijafahamika moja kwa moja kama naye atafunguliwa mashtaka au la”.
