Wanafunzi wachoma moto pikipiki ya mwalimu na kufyeka shamba lake la mahindi

0
24

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Singida, Stella Rutabihirwa amethibitisha kushikiliwa kwa wanafunzi sita wa kidato cha tano na sita Mchepuo wa CBG, kutoka Shule ya Sekondari Mwenge iliyopo Manispaa ya Singida kwa tuhuma za kuchoma Pikipiki ya mwalimu wa shule hiyo na kuharibu mazao.

Akizungumza mkoani hapo amesema kuwa tukio hilo lilitokea Februari 24 mwaka huu saa 5:30 usiku katika eneo la shule hiyo, huku akibainisha kuwa uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa chanzo cha tukio hilo ni mwalimu wa shule kumwadhibu mwanafunzi mwenzao wa kidato cha sita, kwa kosa la kuficha simu aliyokuwa akiimiliki kinyume na taratibu za shule.

Kwa mujibu wa RPC Rutabihirwa mwanafunzi huyo alibainika akiwa ameficha simu baada ya waalimu kufanya upekuzi katika mabweni ya wanafunzi, kwa lengo la kubaini ukiukwaji wa taratibu za shule.

Hata hivyo inadaiwa kuwa wanafunzi hao walikwenda kuchukua pikipiki ya mwalimu huyo iliyokuwa imeegeshwa kibarazani, kisha wakaichoma moto umbali wa mita 150 kutoka nyumbani kwa mwalimu huyo anapoishi, na baadaye wanafunzi hao walifyeka shamba la mahindi lenye ukubwa wa hekari moja analomiliki mwalimu huyo.