Matumaini ya wanafunzi 54 wa Kitanzania waliokuwa wakisoma nchini Sudan na kuhitimu mwaka 2022, yamefifia kutokana na kutopata vyeti vyao vya kitaaluma hadi sasa.
Pamoja na kukamilisha masomo yao kwa bidii, wanafunzi hao wanakabiliwa na changamoto ya kukosa nyaraka hizo muhimu, ambazo ni msingi wa ndoto zao za kupata ajira au kujiendeleza kitaaluma.
Mmoja wa wanafunzi hao kutoka Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Afrika kilichopo Sudan, Semili Pazi, ameelezea masikitiko yake makubwa kuhusu hali hiyo akisema ni jambo la kusikitisha kwa wengi wao kutumia miaka saba kusoma nje ya nchi na kurudi nyumbani bila vyeti vyao muhimu.
“Tulitumia miaka mitano kusomea udaktari, mwaka mmoja tukijifunza lugha, na mwaka mwingine ulipotea kutokana na changamoto za janga la corona. Nilipomaliza mitihani yangu, nilibaki Sudan ili kukamilisha taratibu za kuhitimu na kusubiri vyeti vyangu,” alisema Bw. Pazi.
Hata hivyo, hali ilibadilika ghafla baada ya kuzuka kwa vita mnamo Aprili 2023, jambo lililowalazimu wanafunzi hao kurudi Tanzania bila kupata vyeti vyao. Pazi, ambaye alihitimu Shahada ya Kwanza ya Udaktari mwezi Februari 2023, bado hajapokea hati yake ya matokeo wala cheti cha kuhitimu, ambavyo ni muhimu kwa maombi ya ajira na hatua nyingine za maendeleo.
Changamoto hiyi imewaweka wanafunzi hao katika hali ya kukata tamaa na sintofahamu, huku ndoto zao za kutumia elimu yao kwa manufaa ya taifa zikionekana kuzidi kufifia.
Chanzo: The Citizen