Wanafunzi wanaopata ujauzito ruksa kurejea shule

0
40

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amesema wanafunzi wa shule za msingi na sekondari watakaokatisha masomo yao kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo utoro, mimba na matatizo ya kifamilia watapewa fursa nyingine ya kurejea katika mfumo rasmi wa elimu mara naada ya kujifungua au kumaliza tatizo linalowakabili.

Waziri Ndalichako ametoa kauli hii leo jijini Dodoma akieleza mafanikio ya Sekta ya elimu katika kipindi cha miaka 60, akiongeza kwamba serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuboresha sekta ya elimu.

“Leo natoa waraka wa elimu ambao utaelezea ni lini Wanafunzi watakaokatisha masomo kwa sababu ya mimba na changamoto nyingine watapaswa kurejea shuleni,” amesisitiza Ndalichako.

Ameeleza serikali imeamua Wanafunzi wa darasa la saba wanaofutiwa matokeo kutokana na udanganyifu na wanaoshindwa kufaulu mitihani au wanaopata changamoto zozote wakati wa mitihani yao watapewa fursa ya kurudia mitihani hiyo mwaka unaofuata.

“Utaratibu wa sasa Mwanafunzi anapofutiwa mtihani, anapofeli darasa la saba au kupata changamoto yoyote wakati wa mitihani anakuwa hana fursa nyingine ya kufanya mtihani,” ameleeza.

Ametumia nafasi hiyo kuwaonya watumishi na wasimamizi wa mitihani kuwa wasifikiri kwamba kwa vile kuna marudio kibano kwao kitaondolewa. “Tutaendelea kuchukua hatua kwa wote watakaohusika na udanganyifu wa Mitihani.”

Juni 2021 serikali ilitoa taarifa  kueleza kuwa wanafunzi waliokatiza masomo yao kwa kwa sababu ya kupata mimba watqruhusiwa kurejea masomoni kupitia vyuo vya maendeleo ya wananchi.

Aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati John Magufuli alipiga marufuku wanafunzi wanaopata mimba shuleni kuendelea na masomo ya shule ya msingi na sekondari hali iliyozua mijadala kutoka kwa wanaharakati wa haki za binadamu nchini na nje ya nchi.

Send this to a friend