BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza orodha ya awamu ya tatu yenye jumla ya wanafunzi wapya 3,544 waliopangiwa mikopo kwa mara ya kwanza katika mwaka wa masomo 2020/2021 yenye thamani ya TZS bilioni 11.04.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru amesema ili kupata taarifa za kina kuhusu mikopo waliyopangiwa, wanafunzi hao wanashauriwa kutembelea akaunti zao walizotumia kuomba mikopo kwa njia ya mtandao maarufu kama SIPA – Student’s Individual Permanent Account (SIPA).
“Kufuatia kutolewa kwa awamu hii ya tatu, hadi sasa jumla ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliopangiwa mikopo ni 53,364 yenye thamani ya TZS bilioni 173.29. Aidha, jumla ya wanafunzi 69,625 wanaoendelea na masomo wamepangiwa TZS bilioni 247.5 baada ya kufaulu mitihani yao ya mwaka 2019/2020,” amesema Badru.
Ameongeza kuwa dirisha la rufaa limefunguliwa kwa siku saba (07) kuanzia kesho (Jumatano, Desemba 2, 2020) ili kuwawezesha waombaji ambao hawajapangiwa mikopo au hawajaridhika na viwango walivyopangiwa kuambatisha nyaraka za ziada kuthibitisha uhitaji wao.
Kwa mujibu wa Badru katika kipindi cha rufaa, wanafunzi watahitajika kutembelea mfumo wa olas.heslb.go.tz, kufuata maelekezo na kuwasilisha rufaa zao kutoka popote walipo bila malipo yoyote.
“HESLB inatoa wito kwa wanafunzi ambao bado hawajapangiwa mikopo na ni wahitaji, kutumia muda wa siku saba za rufaa kuwasilisha nyaraka sahihi ili hatimaye wapangiwe mikopo ya kuwawezesha kulipia gharama za masomo,” amesema Badru.