Wanafunzi watano wachoma shule moto na kusababisha hasara ya milioni 26

0
41

Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela amewachapa viboko wanafunzi watano waliochoma moto Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Oswe na kusababisha hasara ya zaidi ya TZS 26 milioni.

RC Mwangela amesema wanafunzi Naftari Nganga na Collin Kisinga ndio waliochoma mabweni ya shule hiyo huku wenzao watatu wakiwa na taarifa za mipango hiyo na hawakuripoti.

Amesema wanafunzi hao walianza mpango wa kuchoma moto mabweni mnamo Juni 28 kwa kununua vifaa vya kuchomea, ilipofika Julai 2 walijaribu kuchoma bweni lakini halikuwaka, Julai 3 walichoma bweni likawaka na kusababisha hasara hiyo na Julai 6 walifanya jaribio lingine tena la kuchoma moto ghala la chakula lakini halikuwaka moto.

Brig. Jen. Mwangela ametoa miezi mitatu kwa wazazi wa Naftari na Collin kila mmoja alipe shilingi milioni 7.3. Pia, Mmiliki wa Shule pia amebainika kuwa na uzembe wa kutoweka vifaa vya kuzimia moto hivyyo ametakiwa kulipa shilingi milioni 7.3 huku mwalimu wa zamu siku ya tukio, mlinzi na patroni nao wakitakiwa kulipa shilingi milioni 4 ili kufidia hasara iliyotokana na ajali hiyo ya moto.

Aidha Brig. Jen Mwangela amewaagiza maafisa elimu wote Mkoa wa Songwe kuhakikisha wanafanya ukaguzi katika shule zote ili kubaini endapo elimu ya tahadhari ya majanga ya moto na vifaa muhimu kwa ajili ya kuzima moto vimewekwa katika maeneo ya shule pamoja na kuzingatia taratibu na miongozo ya uendeshaji wa shule.

Pia amewataka wanafunzi kuzingatia masomo na kuacha tabia za kujiingiza katika vitendo viovu vinavyoweza kuharibu maisha yao kwani taifa linawategemea wawe wananchi bora na viongozi au watendaji wa baadae.

Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Wavulana ya Oswe Fabian Mwalyego amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Songwe kwa kuchukua hatua muhimu katika kukabiliana na janga la moto lililotokea shuleni hapo huku akiahidi kurekebisha mapungufu yaliyobainika katika shule hiyo.

Send this to a friend