Wanajeshi wa Niger wampindua Rais Bazoum

0
25

Rais wa Niger, Mohamed Bazoum amepinduliwa na wanajeshi saa chache baada ya kuwekwa kizuizini na walinzi wake katika Ikulu ya nchi hiyo.

Akisoma taarifa, Kanali Amadou Abdramane ambaye alionekana na maofisa wengine tisa waliovalia sare, amesema vikosi vya ulinzi na usalama vimeamua kusitisha utawala wake kutokana na kuzorota kwa hali ya usalama na utawala mbovu.

Abdramane amesema mipaka ya Niger imefungwa na amri ya kutotoka nje imetangazwa, na taasisi zote za jamhuri zimesimamishwa.

“Taasisi zote nchini zitasitishwa, mipaka imefungwa, na amri ya kutotoka nje usiku kote imeanza, hadi itakapotangazwa vinginevyo,” amesema Kanali huku akionya nchi za kigeni kutoingilia kati sakata hilo.

New Zealand: Waziri wa sheria ajiuzulu baada ya kuendesha gari akiwa amelewa

Mkuu wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) amesema Rais wa Benin, Patrice Talon alikuwa anaelekea Niger katika jitihada za upatanishi, baada ya msukosuko wa hivi punde kulikumba eneo hilo.

Rais Talon alitarajiwa kuwasili Niamey leo kuzungumza na pande zote mbili na kutatua mgogoro huo baada ya mkutano uliofanyika mjini Abuja Jumatano na Rais wa Nigeria, Bola Ahmed Tinubu.

Kiongozi huyo wa Nigeria amesema Rais Talon atafanya upatanishi na walinzi wa Rais na pamoja Bazoum kwa nia ya kupata suluhisho.

Kuchukuliwa kwa madaraka na jeshi, ambayo ni mapinduzi ya saba katika eneo la Afrika Magharibi na Kati tangu mwaka 2020, kunaweza kuongeza ugumu katika juhudi za Magharibi za kusaidia nchi za eneo la Sahel kupambana na uasi wa kijihadi.

Send this to a friend